Benki Ya Maendeleo Ya Kilimo Tanzania (TADB) ikishirikiana na NMB zatimiza azma ya serikali katika kupanua wigo wa huduma za kifedha pamoja na mikopo kwa wakulima wadogo nchini wanaojishughulisha na mazao mbali mbali kama miwa, kahawa, korosho na pamba. Wakizungumza katika mkutano wa wanahabari uliofanyika jijini Dar es Salaam, mkutano uliokuwa na lengo la kurasimisha mikopo kwa wakulima wapatao 2997 wa zao la korosho iliyoyolewa hivi karibuni, ambayo iligharimu zaidi ya shilingi Bilioni 9.3.
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Ndugu Japhet Justine alisema “tulianzisha huduma ya kutoa dhamana ya mikopo kwa wakulima wadogo ambao wasingeweza kukopesheka kirahisi na mabenki ya biashara. Siku hadi siku huduma hii imeleta mapinduzi makubwa. Kwa kushirikiana na NMB pekee tumetoa jumla ya mikopo Bilioni 14.3 kwa AMCOs 32, zenye wakulima 14310.
Akielezea muundo wa huduma ya mikopo ya dhamana Mkurugenzi Mtendaji wa TADB alisema “Ubunifu huu wa mikopo ya dhamana umesaidia mabenki kuwakopesha wakulima wengi zaidi. Hadi sasa tumekwisha kutoa zaidi ya billion 19.7 kwa mabenki manane ambayo tuna mikataba nao ya gurantee scheme. Lengo letu ni kuongeza mikopo ya kwenye kilimo kutoka 8.7% kama ilivyo sasa hadi kufika 15% kwa miaka mitano ijayo” Na kuongeza kuwa benki ya TADB inaamini mfumo wa dhamana utaongeza chachu na kutoa fursa kwa mabenki mengine zaidi kuongeza huduma za mikopo kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo katika kilimo, na kuongeza wigo wa uzalishaji na masoko.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe , alifurashishwa na ubunifu mkubwa unaofanywa na benki ya TADB katika kuchachusha maendeleo ya kilimo nchini alisema “TADB ndio benki inayobeba dhamana ya Serikali kukopesha wakulima, ili benki za biashara ziweze kukopesha wakulima wengi zaidi inahitaji taasisi inayoweza kubeba hiyo dhamana na ndio mana TADB chombo muhimu sana kwetu”
Naibu waziri huyo, alitoa wito kwa mabenki nchini kutatua changamoto za uwekezaji katika miundombinu ya mazao ikiwemo upatikanaji wa ghala za kuhifadhia mazao, kuwa iwapo tutaongeza mikopo na kuwajengea uwezo AMCOs wataweza kufufua maghala yao kwa kuyaboresha yakatumika kibiashara. Vile vile Mhe. Bashe alisisitiza mabenki kuangalia namna ya kupunguza gharama za mikopo ikiwemo kutoa riba nafuu.
Nae Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Ndugu Filbert Mponzi akifunga mkutano huo wa wana habari walisema “tuna Imani kubwa na TADB, ushirikiano wetu umeleta mafanikio mazuri. Ushirikiano huu wa kumuhudumia mkulima umeongeza wigo wa huduma zetu na hadi sasa tumetoa mikopo kwa jumla ya AMCOs 32, zenye wakulima 14,310”.